Zaidi ya wanafunzi 250 wanufaika na elimu ya utunzaji wa mazingira

Zaidi ya wanafunzi 250 wanufaika na elimu ya utunzaji wa mazingira

Na Christina Haule, Morogoro

ZAIDI ya wanafunzi 250 wa shule ya sekondari Uwanja wa Taifa iliyopo Manispaa ya Morogoro wamenufaika na elimu ya utunzaji wa mazingira waliyopewa na Taasisi ya wezesha mabadiliko (WEMA) inayowasaidia kulinda na kutunza mazingira ili kuwaepusha na magojwa ya mlipuko na ya kuambukiza kama vile kipindupindu.

Mkurugenzi wa Taasisi inayojihusisha na kutoa elimu kwa jamii (wezesha mabadiliko, WEMA) Dk.Lusako Mwakiluma alisema kufuatia ongezeko la magonjwa ya mlipuko kwa sasa kama vile U T I na kipindupindu yanayotokana na kuwepo kwa mazingira ya uchafu wameona waitumie nafasi hiyo kutoa elimu kwa wanafunzi hao ili kuifanya shule hiyo kuendeleza usafi na kuwa shule ya mfano kwa shule zingine za Manispaa ya Morogoro

Mkurugenzi huyo alisema pia wamewapatia vifaa mbalimbali vya usafi vyenye thamani ya shilingi milioni moja  ambapo alivitaja vifaa hivyo kuwa ni pamoja na mafagio , brashi za kusafishia vyooni, ndoo za kuwekea maji, plastiki za kuwekea takataka na dawa za kusafishia choo.

Alisema kupitia mradi huo waliouita kwa jina la ‘usiupotezee uchafu’ katika shule za sekondari sababu mazingira safi ni maendeleo ambapo mradi huo waliuanzisha baada ya kufanya tafiti na kubaini kuwa katika shule nyingi za sekondari za kata vyoo vyake ni vichafu ambapo kuanzishwa kwa mradi huo kutasaidia wanafunzi kutunza mazingira kwa kusafisha vyoo vyao kila siku ili kuepukana na magonjwa ya UTI na magojwa ya mlipuko kama kipindupindu.

Mwakiluma alisema wataendelea kutoa elimu katika shule zingine nane za Sekondari za kata na baadae kukagua kama wanaendeleza shughuli za utunzaji wa mazingira huku wakiazimia kutoa tuzo kwa shule itakayoendeleza suala zima la utunzaji wa mazingira.

“.Hatuwezi kuweka plasta kidonda bila ya kukiosha ndio mana tumetoa elimu hii ya utunzaji mazingira kwanza kwa kushirikiana nao kwenye usafi na baadae tukatoa vifaa vya kufanyia usafi” alisema Dk. Mwakiluma.

Naye Mwalimu wa nidhamu wa shule hiyo Asifiwe Charles  alisema vifaa vilivyotolewa na WEMA vitawasaidia wanafunzi kufanya usafi na kutunza mazingira vyema ili kuepukana na magojwa  kwani hapo awali kulikuwa na upungufu wa vifaa kama hivyo shuleni hapo.

Alisema awali shuleni hapo hapakuwa na dastibini za kuwekea  taulo za kike mara baada ya kutumika ambapo wasichana walikuwa  wakibadilisha pedi zao wanalazimika kutupa katika vyoo na kusababisha kuziba kwa vyoo mara kwa mara na kuingia gharama za kuzibua fedha ambazo zingetumika kwa maendeleo mengine ya shule.

Naye Dada Mkuu wa shule ya sekongari Uwanja wa Taifa Irene Mkondya  alisema ataendelea kuwahamasisha wanafunzi wenzie kutunza mazingira kwa maendeleo kwani ameweza kujifunza hasara za kuharibu mazingira kama kutupa taka hovyo kunavyoleta magojwa ya mlipuko kama kuharisha na kipindupindu hivyo aliwasasa wanafunzi wote kutunza mazingira kwani kwa kutunza mazingira watapata maendeleo.

Naye Omari Shabani mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo alisema  elimu waliyopata ya utunzaji wa mazingira itawasaidia katika maisha yao ya kila siku wawapo mashuleni na hata majumbani kwa sababu wanaweza kutunza mazingira kwa maendeleo.

Hivyo aliwasihi wanafunzi kuendelea kutunza mazingira ili kuepukana na magojwa ambayo yanaweza kuwakalisha chini na kuwafanya kushindwa kuendelea na masomo lakini pia kushindwa kuendelea na shughuli zao za maendeleo hapo baadae wakiwa wameshaanza kazi.

Taasisi ya wezesha mabadiliko hutoa elimu ya kujitambua  kwa vijana na wanafunzi, elimu ya afya ya uzazi, jinsi ya  kuepuka mimba na ndoa  za utotoni na jinsi ya kuepuka TB, Ugonjwa wa  upungufu wa kinga mwilini(UKIMWI) na kwamba kwa sasa inatekeleza mradi wa miezi nane katika shule 8 za sekondari za kata zilizopo manispaa ya Morogoro.

WEMA- Yakabidhi Choo cha Mtoto wa Kike

WEMA- Yakabidhi Choo cha Mtoto wa Kike

Choo cha Mtoto wa Kike Shule ya Sekondari Uluguru ,kilichofadhiliwa na Taasisi ya WEZESHA MABADILIKO.

Mkurugenzi wa WEZESHA MABADILIKO, Dr. Lusako Mwakiluma (kushoto), akisalimia na Afisa Elimu Taaluma Msingi Manispaa ya Morogoro, Leah Selemani (kulia) mara baada ya uzinduiz wa Choo cha Mtoto wa Kike.

Mkurugenzi wa WEZESHA MABADILIKO, Dr. Lusako Mwakiluma (watatu kutoka kushoto) , Mtendaji wa Kata ya Kihonda Tatu Ally (kushoto) wakiwa na Wanafunzi mara baada ya uzinduzi wa Choo cha Mtoto wa Kike.

Mkurugenzi wa WEZESHA MABADILIKO, Dr. Lusako Mwakiluma (watatu kutoka kushoto),akimkabidhi ndoo ya kunawia maji Afisa Elimu Taaluma Msingi Manispaa ya Morogoro, Leah Selemani (kulia).

TAASISI isiyo ya Kiserikali ya WEZEESHA MABADILIKO chini ya Mkurugenzi wake. Dr. Lusako Mwakiluma,imeikabidhi Manispaa ya Morogoro Choo cha Mtoto wa Kike katika Shule ya Sekondari Uluguru.

Tukio hilo la makabidhiano ya Choo limefanyika hivi karibuni ambapo Choo hicho katika makabidhiano kilipokelewa na Mwakailishi wa Mkurugenzi kutoka idara ya elimu Msingi, Leah Selemani.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi choo hicho, Mkurugenzi wa WEZESHA MABADILIKO, Dr. Lusako, amesema kwa kuwa wanawake wengi wamekuwa na changamoto nyingi katika mabadiliko ya kimwili hivyo wameona kujenga Choo cha Mtoto itakuwa ni suluhisho la kuwaondolea adha wanafunzi wakike wanapoingia katika hedhi.

Dr. Lusako,amesema kuwa tafiti  zinaonesha kuwa mtoto wa kike anakosa masomo siku 4 hadi 5 kila mwezi kutokana na ukosefu wa huduma ya vyoo bora na maji salama na safi shuleni ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizosaini mkataba wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Miongoni mwa malengo hayo ni lile lengo namba 4: linalohamasisha kuhusu Elimu Bora, Lengo la 5: linalo hamasisha juu ya Usawa wa Kijinsi na lengo namba 6: kuhusu Maji Safi na Salama.

“Huu ni mwanzo tu bado tuna malengo ya kusaidia na shule nyengine ,  tunataka choo hiki kiwe cha mfano katika Manispaa yetu ya Morogoro , tuliona kuna Choo Tubuyu Sekondari lakini kuna chengine hakijaisha pale Kihonda Sekondari, sisi baada ya kuguswa na jitihada hizi, tumeona nasisi  tuunge mkono jitihada za  Manispaa yetu kwa kuwajengea Choo hiki cha Kisasa  ili kuhakikisha mtoto wa kike anawekewa mazingira rafiki anapokuwa shuleni ili aweze kuhudhuria siku za masomo kwa ukamilifu kama ilivyokuwa kwa mtoto wa kiume kwani “Ukimkomboa mtoto wa kike umekomboa Taifa zima” Ameongeza Dr. Lusako.

Aidha, amesema kuguswa kwao katika ujenzi wa Vyoo vya Mtoto wa kike imetokana na changamoto zinazoendelea kuwakabili wanafunzi kukosa vyoo bora na maji salama na safi shuleni. Tatizo hili linawaathiri watoto wa kike zaidi kwani wanashindwa kujistiri hasa wanapokuwa katika siku zao za hedhi katika mazingira ya shuleni.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro,ambaye pia ni afisa Taaluma Msingi,  Leah Selemani, amempongeza Mkurugenzi wa WEZESHA MABADILIKO kwa  kuwasaidia wanafunzi wa kike shuleni.

Amesema Vyoo hivyo vitapunguza utoro kwa watoto wa kike kwani wengi wamekuwa wakishindwa kufika shule wakati wa hedhi lakini baada ya ujenzi huo utasaidia sana na wanafunzi watahuduhuria shule wakiwa katika hali hiyo maana ipo sehemu salama kwao katika kujisafisha na kujilinda.

Mama Selemani , ameowaomba Wazazi kuwahimiza watoto kwenda shule mara baada ya kupata hedhi kwani mabadiliko hayo yanazuilika wakiwa shuleni.

“Dada yetu Dr. Lusako, amefanya jambo zuri sana, sisi kama Manispaa tunampongeza sana kwa jitihada zake, hii ni mbinu nzuri sana , hiki ni choo cha 3 kwa Manispaa yetu, kimoja kipo Tubuyu Sekondari, kingine kipo Kihonda Sekondari hakijaisha na mategemeo yetu kiishe mwaka huu unaokuja wa 2022, choo hiki  kitasaidia kupunguza utoro kwa watoto wa kike wanaoingia katika siku zao (hedhi), kumekuwa na changamoto wanafunzi kubeba pedi kwenye begi na kwenda nazo shule wengine wanaenda kuomba ofisini , lakini kwa hali hii ni vigumu hata kutambua mtu yupo katika hali gani maana vifaa vyote vitakuwa chooni ni yeye kwenda na kujihudumia”Amesema Mama Selemani.