Zaidi ya wanafunzi 250 wanufaika na elimu ya utunzaji wa mazingira

Zaidi ya wanafunzi 250 wanufaika na elimu ya utunzaji wa mazingira

Na Christina Haule, Morogoro

ZAIDI ya wanafunzi 250 wa shule ya sekondari Uwanja wa Taifa iliyopo Manispaa ya Morogoro wamenufaika na elimu ya utunzaji wa mazingira waliyopewa na Taasisi ya wezesha mabadiliko (WEMA) inayowasaidia kulinda na kutunza mazingira ili kuwaepusha na magojwa ya mlipuko na ya kuambukiza kama vile kipindupindu.

Mkurugenzi wa Taasisi inayojihusisha na kutoa elimu kwa jamii (wezesha mabadiliko, WEMA) Dk.Lusako Mwakiluma alisema kufuatia ongezeko la magonjwa ya mlipuko kwa sasa kama vile U T I na kipindupindu yanayotokana na kuwepo kwa mazingira ya uchafu wameona waitumie nafasi hiyo kutoa elimu kwa wanafunzi hao ili kuifanya shule hiyo kuendeleza usafi na kuwa shule ya mfano kwa shule zingine za Manispaa ya Morogoro

Mkurugenzi huyo alisema pia wamewapatia vifaa mbalimbali vya usafi vyenye thamani ya shilingi milioni moja  ambapo alivitaja vifaa hivyo kuwa ni pamoja na mafagio , brashi za kusafishia vyooni, ndoo za kuwekea maji, plastiki za kuwekea takataka na dawa za kusafishia choo.

Alisema kupitia mradi huo waliouita kwa jina la ‘usiupotezee uchafu’ katika shule za sekondari sababu mazingira safi ni maendeleo ambapo mradi huo waliuanzisha baada ya kufanya tafiti na kubaini kuwa katika shule nyingi za sekondari za kata vyoo vyake ni vichafu ambapo kuanzishwa kwa mradi huo kutasaidia wanafunzi kutunza mazingira kwa kusafisha vyoo vyao kila siku ili kuepukana na magonjwa ya UTI na magojwa ya mlipuko kama kipindupindu.

Mwakiluma alisema wataendelea kutoa elimu katika shule zingine nane za Sekondari za kata na baadae kukagua kama wanaendeleza shughuli za utunzaji wa mazingira huku wakiazimia kutoa tuzo kwa shule itakayoendeleza suala zima la utunzaji wa mazingira.

“.Hatuwezi kuweka plasta kidonda bila ya kukiosha ndio mana tumetoa elimu hii ya utunzaji mazingira kwanza kwa kushirikiana nao kwenye usafi na baadae tukatoa vifaa vya kufanyia usafi” alisema Dk. Mwakiluma.

Naye Mwalimu wa nidhamu wa shule hiyo Asifiwe Charles  alisema vifaa vilivyotolewa na WEMA vitawasaidia wanafunzi kufanya usafi na kutunza mazingira vyema ili kuepukana na magojwa  kwani hapo awali kulikuwa na upungufu wa vifaa kama hivyo shuleni hapo.

Alisema awali shuleni hapo hapakuwa na dastibini za kuwekea  taulo za kike mara baada ya kutumika ambapo wasichana walikuwa  wakibadilisha pedi zao wanalazimika kutupa katika vyoo na kusababisha kuziba kwa vyoo mara kwa mara na kuingia gharama za kuzibua fedha ambazo zingetumika kwa maendeleo mengine ya shule.

Naye Dada Mkuu wa shule ya sekongari Uwanja wa Taifa Irene Mkondya  alisema ataendelea kuwahamasisha wanafunzi wenzie kutunza mazingira kwa maendeleo kwani ameweza kujifunza hasara za kuharibu mazingira kama kutupa taka hovyo kunavyoleta magojwa ya mlipuko kama kuharisha na kipindupindu hivyo aliwasasa wanafunzi wote kutunza mazingira kwani kwa kutunza mazingira watapata maendeleo.

Naye Omari Shabani mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo alisema  elimu waliyopata ya utunzaji wa mazingira itawasaidia katika maisha yao ya kila siku wawapo mashuleni na hata majumbani kwa sababu wanaweza kutunza mazingira kwa maendeleo.

Hivyo aliwasihi wanafunzi kuendelea kutunza mazingira ili kuepukana na magojwa ambayo yanaweza kuwakalisha chini na kuwafanya kushindwa kuendelea na masomo lakini pia kushindwa kuendelea na shughuli zao za maendeleo hapo baadae wakiwa wameshaanza kazi.

Taasisi ya wezesha mabadiliko hutoa elimu ya kujitambua  kwa vijana na wanafunzi, elimu ya afya ya uzazi, jinsi ya  kuepuka mimba na ndoa  za utotoni na jinsi ya kuepuka TB, Ugonjwa wa  upungufu wa kinga mwilini(UKIMWI) na kwamba kwa sasa inatekeleza mradi wa miezi nane katika shule 8 za sekondari za kata zilizopo manispaa ya Morogoro.